9 Januari 2023 - 15:17
Rais Ebrahim Raisi: Wamagharibi waliingia Afrika kwa ajili ya kukoloni na kupora utajiri wa Waafrika

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, madola ya Magharibi yaliingia barani Afrika kwa ajili ya kukoloni na kupora maliasili na utajiri wa Waafrika.

Rais wa Iran amesema hayo wakati alipopokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Mali hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, madola ya Magharibi hayakuingia Afrika kwa ajili ya kusaidia bali kwa lengo la kupora mali na utajiri wa bara la Afrika.

Ebrahim Raisi ameongeza kusema kuwa, kwa kuzingatia maliasili na utajiri ulizonazo nchi za Kiafrika sambamba na rasilimali watu zinaweza kupiga hatua kiustawi na maendeleokwa kuwa na mamlaka ya kujitawala na pasi na kuingiliwa na madola ya Maghiri

Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, uwepo wa madola ya Magharibi katika maeneo mbalimbali ya dunia sio tu kwamba, haujawa na faida yoyote kwa amani na usalama, bali umekwamisha na kusababisha ukosefu wa usalama. 

Rais Ebrahim Raisi amesema kwa kuzingatia uwezo mkubwa ulionao Iran, iko tayari kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali ya Kiafrika ikiwemo Mali.

Kwa uapnde wake Mohamed Maiga, balozi mpya wa Mali hapa mjini Tehran amesifu maendeleo makubwa ya kiuchumi ya Iran na kubainisha kwamba, Tehran inatambuliwa katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya kielimu na kisiasa ya Afrika kama moja ya mataifa yenye kuchomoza kiuchumi na hivyo nchi yake inataka kuimarisha uhusiano na taifa hili.

342/